Majambazi 8 Wauwawa na Jeshi la Polisi Mwanza

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kutumia kikosi chake kabambe chenye umahiri na uweledi uliotukuka tumefanikiwa kuwasambaratisha kwa kuwapiga risasi majambazi nane na badae majambazi hao walifariki dunia wakati wakipelekwa hospitali, katika mapambano ya majibizano ya kurushiana risasi kati ya askari na majambazi hao yaliyochukua takribani masaa matatu na kufanikiwa kukamata silaha mbili ambayo ni AK 47 isiyo na namba na short gun moja iliyotengezwe kienyeji na risasi 15 za AK47, huko Wilayani Ukerewe.

Tukio hilo limetokea tarehe 26.01.2019 majira ya saa 01:00hrs hadi saa 03:00hrs usiku, katika daraja linalotenganisha vijiji vya Buhima na Igala, hii ni baada ya kupata taarifa za kiintelejensia kwamba Wilayani Ukerewe kumeingia majambazi wapatao kumi wenye silaha za moto wakiwa na nia ya kupora fedha na vitu mbalimbali kwenye maduka na makazi ya watu mjini Nansio.

Baada ya kupata taarifa hizo polisi tuliweka mtego na kujipanga vizuri ili tuweze kukamata majambazi hao wakiwa hai na baadae tuweze kuwahoji na kubaini mtandao wao. Aidha wakati tunaendelea kujipanga ghafla majambazi hao walitokea na kuanza kurusha risasi kwa askari.

Polisi tulijibu mashambulizi katika mapambano hayo ya kurushiana risasi yaliyochukua masaa matatu na baadae tulifanikiwa kuwapiga risasi majambazi nane ambao walifariki dunia wakati wakipelekwa hospitali huku majambazi wengine wawili wakifanikiwa kutoroka.

Katika tukio hilo Polisi tulifanikiwa kukamata vitu vifuatavyo;
Silaha moja aina ya AK47 isiyo na namba
Silaha aina short gun iliyotengenezwa kienyeji.
Magazine mbili.
Risasi 15 za AK47.
Maganda 23 ya silaha aina ya AK47.
Panga moja.
Nondo moja na
simu sita.

Aidha katika tukio hilo hakuna askari yeyote aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa. Polisi tunaendelea na msako kabambe wa kuhakikisha mtandao wa majambazi hao unatiwa nguvuni. Miili ya majambazi hao imehifadhiwa hospitali ya Wilaya ya Ukerewe kwa ajili ya uchunguzi na utambuzi, pindi uchunguzi ukikamilika itakabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, tunatoa onyo kwa baadhi ya vijana wanaojihusisha na uhalifu kuwa waache kwani ni kosa la jinai lakini pia utagharimu maisha yao. Sambamba na hilo tunaendelea kuwaomba wananchi watupe ushirikiano kwa kutupa taarifa za wahalifu na uhalifu mapema ili tuweze kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

Imetolewa na:
Jonathan Shanna – ACP
Kamanda wa Polisi (M) Mwanza.
26 January, 2019.

SOMA ZAIDI