Misaada kwa waathirika wa tetemeko iwafikie walengwa

WATANZANIA hivi sasa wako katika hali ya mshikamano wa aina yake kukabiliana na janga la tetemeko kubwa la ardhi lililokumba mkoa wa Kagera mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kutokana na janga hilo, tumepoteza maisha ya watanzania wenzetu 17, wengine 253 kujeruhiwa, nyumba 840 kuanguka na nyingine zaidi ya 1,264 zikipata nyufa yakiwemo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma na za kijamii.
Kutokana na uhalisia wa janga hilo linalotukabili, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa juzi alihamasisha wafanyabiashara, mabalozi na wengine wenye mapenzi mema na Watanzania kuchangia wenzetu waliokumbwa na janga hilo ambapo jumla ya Sh bilioni 1.4 zilichangwa.
Sambamba na mchango wa fedha, ilitolewa pia mifuko ya saruji 2,800 na kampuni nyingine zikiwa zimejitolea kujenga shule mbili za sekondari zilizofungwa kutokana na majengo yake kuharibika vibaya kwa tetemeko hilo. Michango zaidi inazidi kumiminika kwa ajili ya kuwasaidia wenzetu wa Kagera, ikiwa ni pamoja na mahema, chakula na dawa.
Tunapenda kuungana na watanzania wenzetu kuwapongeza wasamaria waliotoa michango hiyo na wale wanaoendelea kufanya hivyo kwa lengo moja kubwa la kuwezesha wenzetu waliokumbwa na kadhia hii, warejee katika uhalisia wa maisha baada ya maafa hayo makubwa.
Lakini tunapenda pia kutoa angalizo kwa wenzetu wanaohusika na uratibu wa misaada inayotolewa katika janga hili la tetemeko, kwamba wajitahidi kuweka utaratibu utakaowezesha kuhakikisha kwamba misaada yote ya fedha na vifaa mbalimbali vya kukarabati miundombinu iliyoharibika vinawafikia walengwa na siyo vinginevyo.
Hakuna ubishi kwamba wapo watu ambao kwa hila na tabia zao tu hupenda kutumia maafa kama hayo kuweza kujinufaisha binafsi badala ya walengwa ambao hivi sasa wako katika hali ngumu.
Kutokana na hali hiyo tungependa kuikumbusha Kamati ya Maafa kujipanga sawia kukabiliana na watu wa aina hiyo bila kuwaonea huruma na iwapo watapatikana basi wafikishwe kwenye vyombo vya sheria ili nao wapate wanachostahiki.
Wananchi nao kwa upande wao wawe macho na watu watakaojaribu kuhujumu walengwa na michango hiyo, kwa kutoa taarifa katika vyombo husika kama polisi na viongozi wa serikali ili kwa pamoja kusiwepo mwanya wa kifisadi katika michango hiyo.
Watanznia tuna utamaduni wa kushirikiana na kushikamana katika kukabiliana na majanga na matatizo mbalimbali yanaoikumba jamii yetu hivyo tunaamini pia kwamba kwa janga hili sote tupo tena wamoja kuweza kuwaokoa na kuwafariji kwa uhalisia wenzetu waliofikwa na maafa hayo kwa kuwapatia misaada wanayohitaji na kuhakikisha pia kwamba inawafikia.

SOMA ZAIDI