BAADA YA NICHOLAS GYAN, JOSEPH OMOG AAGIZA MGHANA MWINGINE KUTUA KAMBINI AFRIKA KUSINI


WAKATI mshambuliaji Nicholas Gyan ambaye Simba inakusudia kumsajili kutoka Ligi Kuu ya soka nchini Ghana akitajwa kuondoka nchini humo kuelekea nchini Afrika Kusini ambako wekundu hao wa Msimbazi wamepiga kambi hatari, taarifa zinasema Simba imevutiwa na straika Mwingine kutoka Ligi Kuu ya Ghana. 

Imedokezwa kwamba Gyan ambaye ni mdogo wake mwanasoka wa timu ya taifa ya Ghana, Asamoah Gyan anaondoka nchini Ghana katika wiki inayoanza leo kuungana na wachezaji wengine wa Simba wanaofanya mazoezi nchini huko. 

Imeelezwa kwamba mwanasoka huyo anayeongoza kwa kufumania nyavu katika kikosi cha Ebusua Dwarfs anakwenda Afrika Kusini baada ya kocha mkuu wa Simba Joseph Omog kuagiza apelekwe huko ili kabla ya kumsajili ampime na kuona uwezo wake.

 Lakini katika kuonyesha kwamba Simba imepania kufanya makubwa pia inakusudia kumwongeza katika kambi ya mazoezi nchini humo mshambuliaji mwingine anayecheza katika kikosi cha timu nyingine inayoshiriki Ligi Kuu ya Ghana, timu ya Bechem United aitwaye Amed Toure.

 Mshambuliaji huyo kwa sasa anaongoza kwa mabao akiwa amemwacha Nicholas Gyan aliyekuwa anaongoza hadi wiki iliyopita. 

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Asante Kokoto hivi karibuni aliisaidia klabu yake ya Bechem United kuitandika Bolga Al Stars kwa mabao 4-0 yeye mwenyewe akitandika mabao matatu mguuni mwake.

 “Tunamchukua washambuliaji wawili katika Ligi Kuu ya Ghana na wote ndio wanaoongoza kwa ufungaji wa mabao, kuna mtu tumempa kazi ya kuimfuatilia Toure, amesema ni mmoja wa watu wa kazi anapokuwa karibu na goli,” amesema mmoja wa watoa habari wetu. 

Wakati Nicholas Gyan ni kama ana asilimia 70 ya kutua Simba, kwa upande wa Toure ambaye ni raia wa Ivory Coast aliyezaliwa Burikina Fasso anategemewa naye kujaribiwa katika kambi ya Afrika Kusini. Kama wawili hawa watasajiliwa Simba wataungana na Mghana mwinginwe James  Kotei ambaye ameshaonesha uwezo mkubwa katika Ligi Kuu msimu uliopita huku kipa Daniel Agyei akidaiwa kutemwa rasmi. 

SOMA ZAIDI