Rasta kuanza na Simba

KAMA kuna shabiki wa Yanga aliyekuwa na hofu juu ya kiungo rasta, Kabamba Tshishimbi ‘Papii’ kutua klabuni kwao, apumue tu kwa sasa kwani kila kitu kinaenda sawa na Mkongomani huyo ataanza kazi na Simba kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Simba na Yanga zinatarajiwa kuvaana kwenye mechi ya Ngao ya Jamii, itakayopigwa Agosti 23 na rasta lazima awepo uwanjani.
Rasta huyo aliyefichuliwa kwa mara ya kwanza na Mwanaspoti kuwa atatua Yanga akitokea klabu ya Mbabane Swallows ya Swaziland, alitua nchini wikiendi iliyopita na jana Jumatano mabosi wa Yanga walimpeleka kwa wataalamu ili kumpima afya kabla ya kumpa mkataba asaini. Kazi hiyo ya kusaini inatarajiwa kufanyika leo Alhamisi baada ya majibu wa kiungo huyo mkabaji kuonyesha kila kitu kipo poa.
Kazi hiyo ya kuchukuliwa vipimo ilifanywa na jopo la madaktari wakiongozwa na Dk. Nassor Matuzya, aliyewahi kufanya kazi na benchi la ufundi la Yanga ambaye alifichua kuwa vipimo vya rasta vimetiki katika makundi matatu aliyofanyiwa.
Dk. Matuzya aliyeambatana na mwenzake Dk. Christina Luambano na Daktari wa Viungo, Husna Awadh, alisema kiungo huyo alianza kuchunguzwa juu ya historia ya afya yake kuangalia endapo aliwahi kukumbwa na tukio la kuzimia, kuvunjika na hata mapigo ya moyo kusimama.
Daktari huyo alisema baada ya hapo Papii alifanyiwa uchunguzi wa mwili mzima, kisha kumalizia kuchunguzwa juu ya uwezo wa moyo, mapafu kufanya kazi na pia kuchunguzwa katika mifupa na misuli na kubainika hana tatizo lolote.
“Tumemfanyia vipimo hivyo leo (jana) Jumatano na ninaweza kuthibitisha kuwa yuko sawa kwa upande wa vipimo vyote ambavyo tumemfanyia kwa kufuzu maeneo hayo yote,” alisema Dk Matuzya.
“Kilichotuvutia zaidi ni kwamba tofauti na wachezaji wengine wageni ambao tumewahi kuwafanyia vipimo, huyu anaonekana maungo yake hasa misuli na mifupa hayana rekodi mbaya.”
KUSAINI MKATABA
Kutokana na kupenya kwenye hatua hiyo ya vipimo vya afya, Papii anasubiri kwa sasa ni kusainishwa mkataba mpya na taarifa toka ndani ya klabu hiyo ni kwamba kiungo huyo atawekewa mezani mkataba leo ili asaini.
“Atasainishwa kesho (leo) Alhamisi kwani sehemu kubwa ya makubaliano yapo vema na kama ulivyosikia kapenya kwenye vipimo,” kilisema chanzo cha ndani ya klabu hiyo iliyotwaa mataji 27 ya Ligi Kuu Bara.
Chanzo hicho kilidokeza kuwa Papii atasainishwa mkataba wa miaka miwili kuchukua nafasi ya Justine Zulu anayesitishiwa mkataba.     

SOMA ZAIDI