michezo




Kocha Joseph Omog ambaye ametemwa na klabu ya Simba, hakutaka kuachwa kwa beki mkongwe, Method Mwanjali.

Omog raia wa Cameroon, pia imeelezwa hakutaka kusajiliwa kwa beki mwingine wala kusajiliwa kwa beki Juuko Murshid raia wa Uganda kwa kuwa hakuona kama ana mchango mkubwa katika kikosi chake.

Rafiki wa karibu wa Omog ameiambia SALEHJEMBE kwamba pamoja na kocha huyo kufutwa kazi Simba, lakini kuna makosa mengi sana hayamhusu.

“Umeona hali ilivyo, wachezaji wamemuangusha na huenda wazawa wamechangia sana kwa kuwa si watu wanaojituma.

“Lakini kocha amekuwa hataki mambo mengi na hasikilizwi, hakumtaka Juuko kwa kuwa anaona hajitumi, muda mwingi yuko Uganda na akienda huko anachelewa, haonyeshi juhudi mazoezini na kwenye mechi.

“Kwa upande wa Mwanjali, yeye hakutaka aachwe, maana uchezaji wake bado aliamini una msaada. Pia Simba ina walinzi wengi vijana, ilikuwa rahisi kuisaidia Simba wakiwa na beki mzoefu kama Mwanjali.

“Lakini ameachwa, Juuko asiyemtaka amesajiliwa. Leo timu imefanya vibaya yeye ndiye mwenye lawama. Kuna mchezaji kutoka Msumbiji, naye amesajiliwa, aliomba angalau aone video yake tu, hakutumiwa hadi anafika hapa,” alieleza rafiki yake huyo.

Tayari Omog ameishapewa taarifa ya kufutwa kazi baada ya Mohamed Dewji ‘Mo’ kuandika mtandaoni kuwa hana uwezo lakini angemshauri Omog kupumzika.



Hii ilikuwa ni baada ya timu hiyo kufungwa kwa mikwaju 4-3 ya penalti na kuvuliwa ubingwa wa Kombe la Shirikisho na Green Worries inayoshiriki Ligi Daraja la Pili.

SOMA ZAIDI