Tumia Mbinu Hizi kupata Mtaji wa Biashara.

Habari zako rafiki yangu? Bila shaka unaendelea vyema na gurudumu la kusaka maendeleo yako binafsi. Nikutie moyo kadri utavyotumia muda wako kusaka mafanikio ndivyo kadri utayasogelea mafanikio,usikubali kukata tamaa. Kadhalika usije kuacha hata siku moja kuacha kuingiza kitu kipya kichwani kwako, kwa sababu maarifa ni silaha kubwa ya kukufikisha unakokusudi. Ukiijua hii siri ni lazima utakuwa huru sana. Kila siku tumia dakika walau ishirini kusoma makala moja au mbili utaona jinsi utakavyobadilika kitabia na kujenga tabia za kimafanikio.

Leo nitazungumza juu ya kupata mtaji wa kuendesha biashara unayoitamani kuifanya. Nafahamu watu wengi wanatamani kuanzisha au kukuza biashara zao lakini changamoto kubwa kwao ni wapi watapata mtaji wa kufanya hivyo? Lakini ukweli wa mambo haupo hivyo, mtaji sio tatizo kubwa kiasi hicho. Katika dhana nzima ya biashara, changamoto kubwa huwa ni namna ya kupata wazo bora la biashara na usimamizi wa biashara. Mtaji huwa ni kitu rahisi kati ya hivyo kupatikana. 

Ukitaka kuthibitisha kwamba mtaji sio tatizo kubwa kama unavyodhani, angalia ni watu wangapi kila kukicha wanaanzisha biashara lakini baada ya muda mfupi wanafunga biashara, yaani zinawashinda? Utasema hao changamoto yao ni mtaji? Jibu ni hapana, mtaji walikuwa nao ndio maana walifungua biashara, ila tatizo lao kubwa ni usimamizi wa biashara au hawakuwa na mawazo mazuri ya biashara kulingana na maeneo yao.

Ikiwa tayari una wazo bora la biashara na umejiandaa kwa usimamizi wa Biashara lakini umekosa mtaji, basi wewe fanya yafuatayo ili upate mtaji wa biashara yako:-

Mbinu ya Kwanza, Ungana.  

Hii ni mbinu ambayo imewasaidia wengi sana kuanzisha biashara. Hapa unatafuta marafiki au ndugu ambao mnaweza kuchanga kiasi kidogo kidogo cha fedha na kuanzisha biashara ya pamoja. Mara nyingi biashara huwa inahitaji mtaji mkubwa kidogo kulingana na aina ya biashara husika sasa kwa kuungana mnagawana ule mzigo wa mtaji kiasi kwamba kila mtu anabeba mzigo kidogo tu anaoweza kuubeba.
Ukishapata watu wa kuungana kwa ajili ya kuanzisha biashara, kaeni chini mkubaliane aina ya biashara mtakayoanzisha na namna ya kugawana faida. Mara nyingi faida huwa inagawanywa kwa kuzingatia kiasi cha mtaji mhusika alichochangia. Baada ya kukubaliana mnayaweka katika maandishi, mnasaini mnaanza biashara yenu.

Mbinu ya Pili, Uza Mpango wa Biashara.

Mbinu hii pia inaweza kukusaidia kuanzisha biashara yako. Hapa unatafuta fursa bora ya biashara na kuandaa mpango  unaoonyesha namna biashara hiyo itakavyoendeshwa na kiasi cha faidi kinachoweza kutengenezwa; alafu unatafuta watu wenye mtaji unauza wazo lako ukiwashawishi ni kwa namna gani wakikupa mtaji utaweza kutengeneza faida na uwaonyesha ni kwa jinsi gani na wao watanufaika kwa kukupa mtaji wao. 

Wapo watu wengi wenye mitaji ya pesa lakini hawajui pa kuiwekeza, sasa unapowapelekea mpango huo ni sawa na kuwaonyesha fursa ya kutengeneza pesa zaidi kutokana na pesa zao zilizokaa tu. Njia hii huhitaji mtu mvumilivu na mstahimilivu kwa sababu unaweza kwenda kwa watu kumi mmoja tu ndio akaonyesha kuunga mkono wazo lako.

 Lakini kadri utakavyopeleka wazo lako kwa watu wengi zaidi ndivyo unavyokaribia kufanikisha. Usikatishwe tamaa na mtu mmoja au wawili ambao hawapo tayari kuungana na wewe.

Mbinu ya Tatu, kukopa.

Hii ni mbinu ambayo mara nyingi huwa sishauri sana kuitumia kuanzisha biashara japo ni mbinu nzuri sana kukuzia biashara. Unaweza kuchukua mkopo na kukuza biashara ambayo tayari imeshaanza. Mikopo hii unaipata katika taasisi za kifedha, vikundi vidogo vidogo mtaani au kutoka kwa mtu. Lakini ni lazima uwe mwaminifu sana katika pesa hiyo na kuhakikisha marejesho unayafanya kama ulivyoelekezwa. Pia ni lazima uwe unaifahamu vizuri biashara yako na uwezo wake wa kuwezesha kulipa marejesho ya kila mwenzi.

Mbinu ya Nne, Michango.

Hapa unaweza kupata michango kutoka kwa ndugu au marafiki ili uanzishe Biashara yako. Inawezekanaje watu wanachangisha michango ya harusi na wanapata mamilioni ya pesa lakini ishindikane kuchangisha pesa ya mtaji wa biashara? Amu, andaa form andika kichwa cha habari juu mfano “mchango kwa ajili ya kufungua Biashara ya duka”, tembeza fomu yako kwa ndugu zako wa karibu na marafiki zako wachangishe, utashangaa utakavyopata pesa ambayo hukuwa nayo.
Kikubwa hapa, wakati unachangisha usichoke fanya kama unafuatilia kadi ya harusi, wanaochangisha kadi za harusi huwa hawachoki mpaka wamefanikiwa. Anza mara moja, na anzisha biashara yako.

Mbinu ya Tano, Mali kauli.

Hii ni mbinu nyingine ya kufungua Biashara yako. Hapa unaenda kwa wenye maduka unakubaliana nao wanakupa mzigo wa vitu ili uviuze, mnakubaliana kiasi cha pesa utakachokirejesha kwake ili cha juu kiwe ni faida kwako. Baada ya hapo unaunza bidhaa hizo, kiasi kitachopatikana juu ya bei unakichukua na kukitunza baada ya muda fulani utajikuta una kiasi fulani cha pesa ambacho utakitumia kama mtaji wa kununulia bidhaa zako baadaye.

Asante, naomba niishie hapo kwa leo mpaka kesho. Weka uliyoyasoma kwenye matendo na furahia matokeo. Endelea kupata maarifa muhimu kwa maisha yako. Usiache kupata maarifa mapya kila siku.

Ni mimi mwalimu na rafiki yako,
Alex Mushi
alexmushi@rocketmail.com

soma zaidi kwa kubofya hapa akonewstz.blogspot.com

SOMA ZAIDI