Marekani na Korea Kaskazini nini kimebadilika chini ya Trump?

Picha ya Kim Jong-Un iliyopigwa April 15, 2017



Baada ya wiki za majibizano makali kati ya Marekani na Korea Kaskazini, Rais wa Marekani Donald Trump amesema anaweza kufurahia kukutana na Kim Jong Un. Lakini ilikuwaje hadi mambo yakafikia hapa?

Nini kimebadilika chini ya Trump?

Tishio: Wamarekani wanaamini kwamba Korea Kaskazini tayari ina teknolojia ya kurusha makombora ya nyuklia hadi Japan na Korea Kusini. Wanakadiria kwamba taifa hilo litakuwa na uwezo wa kurusha makombora hadi Marekani katika miaka michache ijayo.
Kwa hivyo, Korea Kaskazini kwa sasa inachukuliwa kama tishio kwa usalama wa taifa la Marekani, na si tishio tu kwa washirika wake Asia mashariki. Hii ndiyo inayoongeza dharura katika haja ya kushughulikia tishio hilo.
Maneno makali: Hatua ya kijeshi ndiyo ambayo imefikiriwa zaidi kwa muda mrefu. Lakini hakuna serikali ya Marekani ambayo imekuwa wazi kuhusu hilo kuliko serikali ya Trump. Hii sana ni kutokana na mtindo wa uongozi wa Bw Trump na imani kwamba tishio la Korea Kaskazini limezidi.
Ubabe wa kijeshi: Majira ya kuchipuza huwa ya wasiwasi sana rasi ya Korea, sana kwa sababu ndio wakati Korea Kaskazini husherehekea siku muhimu katika taifa hilo. Ni kipindi hiki ambapo taifa hilo hufanyia majaribio silaha mbalimbali. Aidha, wakati huu pia ndio Marekani hufanya mazoezi ya kijeshi ya pamoja an Korea Kusini.
Lakini mwaka huu, utawala wa Trump umeongeza nguvu katika kuonyesha ubabe wake kijeshi, kwa kutuma nyambizi yenye uwezo wa kurusha makombora pamoja na meli kubwa ya kubeba ndege za kivita. Kulikuwa na utata kuhusu wapi meli hiyo kubwa ilikuwa inaelekea awali, lakini baadaye ilithibitishwa kwamba ilikuwa inaelekea rasi ya Korea. Utata huo huenda ulichangia kupunguza uwezo wake kama onyo kali kwa Korea Kaskazini.











Helikopta ya kijeshi aina ya MH-60R Sea Hawk ikipaa kutoka kwa meli ya USS Carl Vinson 24 April 2017
Helikopta ya kijeshi aina ya MH-60R Sea Hawk ikipaa kutoka kwa meli ya USS Carl Vinson 


 
Korea Kaskazini: Pyongyang kwa muda mrefu imeamini kwamba inahitaji silaha za nyuklia ili kujilinda, na imekuwa tayari kukabiliana na vitisho na adhabu kutoka kwa jamii ya kimataifa.
Kim Jong Un ameonyesha kujitolea kwake, kinyume na babake na babu yake, kupuuza msimamo na maoni na mshirika pekee mkuu wa Korea Kaskazini, China.
Kiongozi wa mashauriano wa zamani wa Marekani Chris Hill anasema Kim Jong il (babake Kim Jong-un) alijali sana yale ambayo wengine walifikiria, na hasa Wachina. Lakini mwanawe Kim Jung Un hajali wasemayo watu.
China: China imeonekana kutamaushwa na mshirika wake Korea kaskazini na ina wasiwasi kuhusu taifa hilo kuendelea kujiimarisha kwa silaha.
Tayari China imeanza kukaza vikwazo vilivyowekewa Pyongyang na Umoja wa Mataifa, sana kuhusu uagizaji wa makaa ya mawe.
Lakini labda ina wasiwasi zaidi kwamba kujionyesha kijeshi kwa Trump kutazidisha uhasama na wasiwasi eneo hilo.
Aidha, China haijafurahishwa na hatua ya Trump kuendelea kukariri kwamba Beijing ina nafasi ya kipekee ya kuweza kuidhibiti Pyongyang.
Katika kilichoonekana kama hatua ya kujibu shinikizo kutoka kwa Marekani, magazeti ya China yalichapisha taarifa zenye msimamo mkali dhidi ya Korea Kaskazini.
Kumekuwa pia na ushirikiano wa karibu zaidi kati ya Beijing na Washington.
Waziri wa ammbo ya nje wa Marekani Rex Tillerson anasema Beijing ametishia kuiwekea vikwazo vyake binafsi Pyongyang iwapo itafanya jaribio la sita la silaha za nyuklia.


Uwezo wa makombora ya Korea Kaskazini

SOMA ZAIDI